WASICHANA WANNE WABAKWA NA KUNDI LA WANAUME WENYE SILAHA

0

 

Baadhi ya washiriki wa maandamano makubwa kulaani vitendo vya ubakaji nchini India
Msako wa nchi nzima umeanza nchini India baada ya wasichana wanne wadogo kutekwa nyara kutoka kwenye nyumba ya kulelea watoto nchini humo na kubakwa na kundi la wanaume wenye silaha wapatao 20.

Wapelelezi walisema kundi hilo la watekaji wenye silaha waliizingira hosteli hiyo iliyoko kijiji cha Lawada katika wilaya ya Pakur na kuwanyaka wasichana wanne wadogo, wote wakiwa na umri wa kati ya miaka 12 na 14.

Mratibu wa polisi, Y.S. Ramesh aliwaeleza waandishi wa habari kwamba wasichana hao, ambao ni kutoka kabila la Paharia, wanatibiwa kwenye hospitali moja ya karibu.

Alisema watuhumiwa hao wamejificha na wanawindwa na polisi kila kona ya nchi hiyo.

Ni tukio la hivi karibuni kabisa la mfululizo wa kesi za ubakaji ambazo zimetikisa kote nchini India katika miezi ya hivi karibuni, na kuibua maswali katika jamii yote ya kimataifa kuhusiana na wanavyotendewa wanawake nchini humo na kupelekea kubadilishwa kabisa kwa sheria zinazohusu makosa ya ubakaji.

Limekuja siku kadhaa baada ya mwanafunzi wa kike wa chuo mwenye umri wa miaka 20 kubakwa na kundi kisha kuchomwa moto huko Etawah, Uttar Pradesh, mji wa jimbo anakotokea Waziri Mkuu Akhilesh Yadav.

Katika tukio hilo, kwa namna ya kushitusha, polisi hao si tu kwamba mwanzoni waligoma kufungua kesi lakini pia walionekana kukwepa majukumu yao ya kusimamia sheria na utii.

Viongozi hao wa juu wa polisi walionesha kutokuwa na msaada katika kukomesha ongezeko hilo la matukio ya ubakaji katika taifa hilo, ambapo yameripotiwa mashambulizi kama hayo 126 wiki iliyopita pekee. Matukio 20 kati ya kesi zote, waathirika waliuawa.

Katika mji mkuu wa Delhi imebainika wiki iliyopita kwamba kumekuwa na kesi 806 za ubakaji zilizoripotiwa katika kipindi cha miezi sita tu mwaka huu, sawa na zaidi ya kesi nne kwa siku, kulinganisha na kesi 706 zilizorekodiwa kwa mwaka mzima wa 2012.

Wakati huohuo, Mahakama kuu ya India itatoa hukumu baadaye mwezi huu katika kesi iliyobeba umaarufu ya tukio la ubakaji la mwanamke ndani ya basi mjini New Delhi ambao walimtupa na kumtelekeza afe kando ya barabara Desemba, mwaka jana.

Hukumu hiyo itakuwa ya kwanza katika kesi za ubakaji, ambayo ilisababisha maandamani ya hasira mitaani nchini India na kushinikiza mabadiliko makubwa kwa sheria za ubakaji nchini humo.

Mwanasheria Rajesh Tiwari aliwaeleza waandishi nje ya mahakama hiyo kwamba mteja wake atafahamu hatima yake Julai 25. Mtuhumiwa huyo alikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo wa shambulio hilo.

Anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha miaka mitatu kwenye kituo cha kurekebisha tabia. Mahakama imeamuru kufichwa kwa jina lake japo tayari ameshatimiza umri wa miaka 18.

Mtuhumiwa huyo ni kati ya watu sita wanaotuhumiwa kuwashambulia mwanamke na mpenzi wake ndani ya basi ambalo lilishamaliza ratiba zake Desemba 16, mwaka jana.

Mwanamke huyo alifariki kwenye hospitali moja nchini Singapore wiki mbili baadaye kutokana na majeraha makubwa.

Washitakiwa wengine wanne wanashitakiwa kwenye mahakama maalumu mjini New Delhi na wanakabiliwa na hukumu ya kifo. Mtuhumiwa wa sita alikutwa amekufa ndani ya kizimba chake gerezani Machi, mwaka huu.

0 comments: