MAREKANI YATOA ONYO KALI KWA MSAFARA WA RAIS OBAMA.

0

Dar es Salaam. Licha ya ujumbe wa Rais wa Marekani, Barrack Obama kutarajiwa kufikia katika hoteli kubwa zenye hadhi wakati kiongozi huyo atakapowasili nchini Julai Mosi mwaka huu, Ikulu ya Marekani imetoa tahadhari ya vyakula ambavyo hawatakiwi kuvigusa wakiwa nchini ikiwa ni pamoja na kutumia maji ya bomba.
Mbali na tahadhari hiyo, ziara hiyo ya Obama itakuwa na ulinzi mkubwa ambao pengine haujawahi kutokea katika historia ya viongozi wa nje wanaotembelea Tanzania kwani utahusisha idadi kubwa ya magari, ndege za kijeshi na meli kubwa ya kivita ambazo zitakuwa zikifanya doria karibu na pwani ya Tanzania.
Tahadhari za matumizi ya chakula, maji na nyinginezo zimetolewa katika nchi zote tatu za Afrika ambazo Obama atatembelea, kila moja kwa jinsi Wamarekani hao wanavyoitathmini.
Rais Obama atatembelea nchi za Tanzania, Senegal na Afrika Kusini.
Ulinzi
Vyombo vya usalama vya Marekani vimejipanga kuhakikisha ziara ya kiongozi huyo haivurugwi kwa namna yoyote ile. Tayari ndege za jeshi zilizobeba magari ya akiba 56, yakiwemo 14 aina ya ‘Cadillac One’ maalumu kwa ajili ya kiongozi huyo, yamewasili katika nchi hizo tatu za Afrika atakazotembelea.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post la Marekani, ndege hizo pia zimebeba malori matatu ambayo yamesheheni karatasi maalumu za kuzuia risasi kupenya kwenye vioo, zitakazobandikwa kwenye madirisha ya hoteli ambazo Rais Obama na ujumbe wake watafikia.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mamia ya mashushushu wa Marekani tayari wako katika nchi hizo. Meli maalumu za kubeba ndege za kivita, maarufu kwa jina la ‘amphibious ship,’ ikiwa na hospitali maalumu na yenye vifaa vyote itaweka nanga baharini, jirani na nchi atakayokuwa Rais Obama, tayari kukabiliana na dharura yoyote itakayotokea. Gazeti hilo liliandika kuwa ndege za kivita za Marekani zitakuwa zikipeana zamu kufanya doria kwa saa 24, katika anga la nchi ambayo Rais Obama atakuwepo, iwapo ndege za ‘adui’ zitakaribia eneo linaloitwa ‘anga ya rais.’ Kwa mujibu wa gazeti hilo, ziara ya Rais Obama aliyoifanya hivi karibuni katika nchi za Ujerumani na Ireland Kaskazini, japo kulikuwa na gharama kwa walinzi, lakini safari za nchi za Afrika zimeelezwa kuwa na gharama kubwa zaidi.
Tahadhari
Kwa mujibu wa taarifa ya maelekezo ya Ikulu ya Marekani, ambayo Mwananchi imepata nakala yake, watu watakaokuwa kwenye msafara wa Obama wametakiwa kutotumia kachumbari. Pia imewataka kutumia maji ya chupa zaidi.
“Kutokana na mfumo wa maji uliopo, tunashauri watu wetu kutumia maji ya chupa zaidi kwa kunywa na hata kwa kupiga mswaki,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa kuelewa fika tatizo la ugonjwa wa malaria nchini, ujumbe wa Obama umeshauriwa kutumia dawa ya mbu ya kupaka na kupuliza inayoitwa Deet.
Deet ni dawa maarufu huko Marekani na ikiwa katika aina tofauti ikiwamo ya kupaka na kupuliza na imekuwa ikitumiwa na jeshi la Marekani kwenye vita mbalimbali tangu miaka ya 1940 kabla ya kuanza kutumiwa na raia mwaka 1957.
ATM nazo noma
Pia watu watakaokuwa kwenye msafara wa Rais Obama wametakiwa kuhakikisha wanatumia mashine za kutolea fedha (ATM) zilizoko karibu na hoteli watakazofikia.
“Kuna tatizo la uhalifu kwa hiyo siyo vizuri kutumia ATM ambazo ziko katika sehemu zisizo salama. Pia katika kipindi watakachokuwa Tanzania watu wanapaswa kutumia teksi ambazo zimeidhinishwa na hoteli.
“Pia siyo vizuri kuacha kompyuta ya fedha kwenye vyumba mtakavyolala. Pia kina mama wanapaswa kuchukua tahadhari ya mabegi yao watakapokuwa wanapita mitaani,” ilitahadharisha taarifa hiyo.

Ratiba ya ziara ya Obama - kukaa siku mbili
Dar es Salaam. Ikulu ya Marekani na Idara ya Habari (Maelezo), wametangaza ratiba ya Rais Barrack Obama atakapozuru Tanzania huku ikionyesha kuwa atakaa siku mbili tu, kuanzia Julai Mosi na kuondoka kesho yake.
Tanzania itakuwa nchi ya mwisho ya Afrika kutembelewa na Obama baada ya Senegal na Afrika Kusini. Mara atakapowasili na ndege yake kubwa ya Air Force One, Rais Obama atazindua barabara mpya katika upande wa Mashariki wa geti la kuingia Ikulu.
Rais Obama, ambaye atafuatana mkewe Michelle pia siku hiyohiyo atazungumza kwa nyakati tofauti na wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika na Marekani kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam.
“Pia amepanga kuzungumza na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,” ilisema taarifa ya Maelezo.
Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria dhifa ya taifa atakayoandaliwa Ikulu na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete. Siku itakayofuata ataweka shada la maua kwenye sehemu ulipokuwa Ubalozi wa Marekani ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliofariki katika shambulizi la bomu mwaka 1998. Pia atatembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion na atatoa hotuba akizungumzia mikakati ya Marekani ya kulisaidia Bara la Afrika kuzalisha nishati ya umeme.
“Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani,” alisema Ofisa wa Ikulu ya Marekani, Ben Rhodes wakati alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika Ikulu ya Marekani kuhusu ratiba ya ziara ya Obama barani Afrika.
Pia mke wa Obama atakuwa na ratiba yake. Julai Mosi, atapata staftahi na mwenyeji wake, Salma Kikwete katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Dar es Salaam.
Pia atatembelea sehemu ubalozi wa zamani wa Marekani na baadaye atashuhudia onyesho la utamaduni la Kikundi cha Baba wa Watoto, ambacho kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 18 kwenye Makumbusho ya Taifa. Julai 2, atahudhuria mkutano na wake wa marais wa nchi za Afrika ambao pia utahudhuriwa na mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush, Laura.

0 comments: