TFDA: MAFUTA YA UBUYU NI HATARI KWA AFYA YAKO

0

Mafuta ya Ubuyu ambayo yamejitwalia umaarufu siku za karibuni kiasi cha kufanya yawe ya bei mbaya sana yameelezwa kuwa si salama kwa afya..
baobab oil
TFDA wamepiga marufuku kwa kuwa yana Tindikali ya mafuta, na anayekunywa kwa wingi ana hatari ya kupata Kansa za aina mbali mbali.

TDFA inaonya jamii kuwa mafuta hayo si mazuri na si salama na inashauri watanzania kuacha kutumia.

HABARI KAMILI HII HAPA KUTOKA HABARI LEO

Imechapishwa Jumatatu, 08 Julai 2013
00:50
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko

BAADA ya kuonya wananchi wanaotumia
dawa za tiba mbadala ambazo
hazijathibitishwa, Mamlaka ya Chakula na
Dawa Tanzania (TFDA), sasa inawataka
wananchi kuacha kutumia mafuta ya ubuyu
kwa kunywa kama dawa.

Akizungumza na gazeti hili juzi katika
Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam, msemaji wa TFDA,
Gaudensia Simwanza, alisema Mamlaka
hiyo ilipima na kubaini mafuta hayo yana
tindikali ya mafuta.

Alifafanua katika maonesho hayo maarufu
kama Sabasaba yanayoendelea katika
viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, kwamba
mafuta hayo hayafai kuliwa na binadamu na
anayekunywa kwa wingi, yuko hatarini
kupata saratani za aina tofauti tofauti.

“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la
wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu
kama dawa, kwa kuwaelekeza wananchi
kunywa. Napenda kuwataarifu kuwa mafuta
hayo ni hatari kwani yana tindikali ya
mafuta,” alisema.

Gazeti hili lilipata sampuli ya vielelezo vya
matumizi yake na manufaa yake mwilini,
kama inayotangazwa na wajasiriamali katika
maeneo mbalimbali na hata katika
mitandao.

Matangazo
“Ni mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu
{au kokwa}. Hukamuliwa kiini chake na
kutoa mafuta. Yana ubora kuliko mafuta
mengine ya kupikia, yana Vitamin A, B, C, D
na F. Pia yanatibu magonjwa mbalimbali,”
kielelezo kimoja kilinadi ubora wake katika
mitandao ya jamii.

Mafuta hayo yamedaiwa kutengeneza seli
zote ndani ya mwili, kuzuia ngozi isiharibike
wala kupata makunyanzi, kuondoa mafuta
ndani ya mishipa ya damu na yanapunguza
uzito uliozidi.

Pia inadaiwa yanarutubisha ini na figo,
yanaleta hamu ya kula, yanaimarisha
mifupa, kucha na nywele, yanaongeza kinga
ya mwili (CD4), yanaondoa sumu na
yanatengeneza sukari iwe katika kiwango
kinachotakiwa.

Maelezo hayo yameendelea kusifu kwamba
yanasaidia kuona vizuri na kujenga
kumbukumbu, yanapunguza vitambi na
matumbo makubwa, yana virutubisho vyote
vinavyohitajika mwilini.

Katika ngozi yametajwa kuondoa madoa,
chunusi, fangasi, upele, mba na muwasho,
yanafaa kwa walemavu wa ngozi (albino).
Pia huondoa hamu ya kutumia dawa za
kulevya na kuponyesha vidonda vya tumbo.
“Endelea kutumia mafuta bora ya ubuyu, ni
bidhaa asilia ya kitanzania. Ni mafuta
yasiyochanganywa na kitu chochote, ni
mafuta asilia,” yamesifiwa katika maelezo
hayo.

Kisukari

Mtumiaji ameelezwa kama ana ugonjwa wa
kisukari, atumie kijiko cha chakula kimoja
tu. Anatakiwa kutumia dozi hiyo ya kwanza
nusu saa kabla ya kula chochote kwa muda
wa siku 15.

Dozi ya pili na ya tatu kwa wagonjwa hao,
inatakiwa kufuata baada ya siku 15 kisha
mgonjwa apumzike wiki moja, huku
akiendelea kupima kila wiki. Kipimo hapo
ni cha hospitali.

Vidonda vya tumbo, figo, ini

Kwa wagonjwa wa vidonda vya tumbo, figo
na ini, wameelekezwa na wajasiriamali hao
kunywa kijiko cha chakula kimoja asubuhi
kabla ya kula chochote, na usiku kijiko cha
chakula kimoja kabla hajala chochote kwa
muda wa siku 15 kwa dozi ya kwanza.
Baada ya hapo, mgonjwa anapumzika wiki
moja kisha siku 15 zinazofuata dozi ya pili,
mapumziko wiki moja halafu siku 15
nyingine dozi ya tatu.

Maelezo ya dozi hiyo ya kutibu ugonjwa wa
vidonda vya tumbo, yanaendelea kumtaka
mgonjwa baada ya dozi ya tatu, aanze
kunywa kila wiki mara moja kijiko cha
chakula kimoja asubuhi, tena nusu saa kabla
hajala chochote kwa muda wa wiki nne.
Dozi inaendelea ambapo mgonjwa
atatakiwa kunywa kijiko kimoja cha chakula
kila mwezi mara moja asubuhi, kabla hajala
chochote kwa muda wa wiki nne, kisha
kunywa kila mwezi mara moja, asubihi
kabla hajala chochote kwa muda wa miezi
sita mfululizo.

Utoaji sumu, CD4

Kwa utoaji wa sumu, mgonjwa ametakiwa
kunywa kijiko cha chakula kimoja asubuhi
kila siku kwa muda wa siku 14, kisha
kunywa kila mwezi mara moja kwa muda
wa miezi sita mfululizo.

Kwa kuongeza CD4 mwilini, ametakiwa
kupata kijiko cha chakula kimoja asubuhi
nusu saa kabla ya kula chochote, na usiku
kijiko cha chakula kimoja nusu saa kabla ya
kula chakula cha usiku kwa muda wa miezi
mitatu.

“Mgonjwa aanze kunywa baada ya kipimo
cha mwisho (cha CD4) alichopima. Mafuta
yanapatikana kuanzia ujazo wa lita moja na
zaidi,” imesifiwa dawa hiyo.

Onyo

TFDA imeonya kuibuka kwa tabia ya
wananchi kutaka matibabu ya haraka, kama
ilivyo kwa baadhi ya watu kutaka utajiri wa
haraka, na imehadharisha ni vema kabla ya
kutumia dawa zinazoibuka kila siku, waulize
kama zina ubora kwa afya zao.

“Nawasihi wananchi kuacha kukimbilia dawa
ngeni mara tu baada ya kutangazwa… kama
haya Mafuta ya Ubuyu, yamekuwa
yakielezwa ni dawa na wajasiriamali tu, na
wengi wamekuwa wakitumia bila kusikiliza
mamlaka husika zinasemaje,” alisisitiza.
Semwanza alisema Mamlaka hiyo iko katika
mkakati wa kuanza kuelimisha jamii kuhusu
matumizi ya mafuta hayo, ambayo wengi
wanayaamini na kuyanywa kama dawa.

Teknolojia, matumizi sahihi

Kwa mujibu wa Semwanza, baada ya
kupima mafuta hayo na kubaini hatari hiyo,
waligundua pia inawezekana tindikali hiyo
kutenganishwa na mafuta hayo, lakini
imebainika utaalamu na teknolojia hiyo
haipo nchini.

Hata hivyo, alisema Mamlaka hiyo
haijabaini madhara ya matumizi mengine
ya mafuta hayo kama kipodozi.

Msako Sabasaba

Kutokana na mvuto huo wa kibiashara, na
shauku ya kupona haraka ya wananchi,
Semwanza alisema TFDA imekuwa ikifanya
msako wa dawa mbalimbali zinaouzwa na
wajasiriamali katika maonesho hayo.

Alisema kuwa kuna baadhi ya waandaaji
wanaowaalika wajasiriamali bila kufuata
kanuni na sheria za kuingiza dawa hizo
katika maonesho.

Kwa mujibu wa Semwanza, wanakagua dawa
na kama wakikuta hazijathibitishwa na TFDA
na mamlaka nyingine, wanamuamuru
mjasiriamali kuacha kuzitangaza mpaka
apate kibali na kuwaasa wanaowaleta
wajasiriamali katika maonesho hayo ya
kimataifa kuhakikisha wanafuata vigezo.

Wiki iliyopita TFDA, ilionya wananchi dhidi
ya matumizi ya dawa za tiba mbadala,
zikiwamo zinazokuza maumbile, ambazo
bado hazijasajiliwa na Mamlaka hiyo baada
ya kuchunguza usalama, ubora na ufanisi wa
dawa hizo.

Mamlaka hiyo ilieleza kuwa, ilitoa nafasi ya
watoa tiba mbadala kwenda kusajili dawa
zao, lakini mwitiko umekuwa hafifu.

TDFA yenye dhamana ya kusimamia ubora
na usalama wa bidhaa za vyakula na dawa,
ikiwa ni pamoja na dawa za mitishamba,
vipodozi na vifaa tiba vinavyouzwa katika
soko la Tanzania, imeeleza kuwa watoa
huduma wa tiba mbadala, wengi hawako
tayari kubainisha aina ya mchanganyiko wa
dawa hizo jambo ambalo ni hatari kwa
walaji
baobab oil

0 comments: