INASIKITISHA: Wanandoa wanavyoshiriki kuua, kutupa watoto Tarime

0

 
Tarime. Waswahili husema, mapenzi matamu pale yanapokolea, lakini hugeuka shubiri pale yanapochacha.
Ukweli wa mambo hayo unadhihirika katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tarime

mkoani Mara ambako imebainika kuwa idadi kubwa ya wanawake, wasichana wanaotoa mimba au kuua watoto wanaowazaa ni kwa sababu ya mapenzi au kukubaliana na wenzi wao.
Wengine huwanyonga, kuwatupa vichanga au watoto wadogo kwa sababu ya kuchuja mapenzi au kwa sababu wamekubaliana na wenza wao wawaue watoto labda kwa sababu hawafanani na mume.
Ukosefu wa uaminifu kwa wapendanao, hususan waliomo kwenye ndoa imekuwa ni sababu ya wahusika kukata tamaa, jambo ambalo limesababisha watoto wanaozaliwa kufanyiwa ukatili na hata kuuawa.
Utafiti uliofanywa katika wilaya hiyo umebaini kuwa watoto wengi wanaozaliwa na kutupwa ni wale ambao wazazi wao ama wapo kwenye ndoa au uchumba, ambao watu wake hawaelewani.
Kwa upande wa wanawake, yule aliyekuwa na uhusiano na mwanamume mwingine na kwa bahati mbaya akapata ujauzito nje ya ndoa hujikuta akilazimika kutoa mimba au kutupa mtoto pindi anapojifungua ili kunusuru ndoa au uchumba.
Kadhalika, mwanamume anapomuhisi mkewe kuwa alikuwa na uhusiano ya kimapenzi na mwanamume  mwingine, ajifunguapo mtoto, humshawishi mke au au yeye huwadhuru wote kwa pamoja.
Pia, mama akishajifungua na baba akaona mtoto hafanani naye, humshawishi mama kumuua mtoto. Matendo haya jambo yanaonekana kupigiwa kelele mno na vyombo vya dola, bado yanaendelea kwa siri kubwa katika baadhi ya maeneo.
Ushuhuda na hali halisi
Ipo mifano kadhaa ya matukio kama hayo kwani wilayani Musoma mwaka 2011, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Robert Boazi ambaye kwa sasa yuko Kilimanjaro aliwahi kuwakamata wazazi ambao walishirikiana kuua mtoto na kisha kumtupa.
Kisa ni nini ?
Ni baada ya baba kudai kuwa mtoto yule aliyezaliwa si wake, bali mwanamke alipewa uja uzito na mwanamume mwingine.
Sufiani Mageta, ambaye ni Katibu wa Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime anasema kuwa wao hupokea watoto wachanga wanaotupwa baada ya kuzaliwa, baadhi yao hukutwa wakiwa hai na wengine wakiwa tayari wamekufa.
Anasema kwa mwaka jana pekee, watoto watatu hai waliokotwa wakiwa wametupwa na sasa wanalelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo mjini Musoma.
Askofu Isaac Kitongo wa Kanisa la Jeshi la Wokovu, Divisheni ya Tarime anasema kuzaa mtoto nje ya ndoa husababisha baadhi yao kutelekezwa.
 Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Magreth Segu anasema: ”Wanaume wa siku hizi wengi, wao wanakataa kuishi na mtoto wa kambo,  hata wakiishi nao wanawanyanyapaa na wengine wamefikia hatua ya kuwaua kwani anaona ni aibu kwa rafiki zake kuwa ameoa mwanamke mwenye mtoto”.
 Abel Gicheina, Ofisa wa Ustawi wa Jamii katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime anasema: “Siku hizi wengi wanaonekana wanaingia kwenye uhusiano kwa kuwa na tamaa zaidi ya upendo wa kweli”.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Tarime, Mwasiti Itumbo anasema kuwa zaidi ya kesi 20 zimeripotiwa mwaka jana ofisini kwake na zote zinazohusu  wanandoa kutoka nje ya ndoa na tatizo la wanaume kutokutoa huduma ya matunzo kwa watoto wanaowazaa.
Itumbo anasema kuwa wanaume hudai kuwa hawatoi matunzo kwa watoto wanaozaliwa kwani wanakuwa si damu yao.
Wanawake kwa upande wao, wanajitetea kuwa wanatoka nje ya ndoa kutokana na baadhi ya wanaume kutotoa matumizi ya kutosha kwa familia zao, badala yake  wengi wao huwajali zaidi wanawake wa nje ya ndoa.
Ingawa si wote wenye tabia hii ya kutoka nje ya ndoa, jambo hilo, ofisa huyo anasema  ndilo linalowafanya  wanawake nao watoke nje ya ndoa  kutafuta watu wa kuwapa mahitaji, baadhi yao hujikuta wamepachikwa uja uzito nje ya ndoa.
 Lucy John, mkazi wa Tarime (si jina lake halisi) anasema kuwa baadhi ya  wasichana ambao hawajaolewa wakiwamo wanafunzi  wanasema kuwa wataacha kutoa mimba iwapo wanaume wanaowabebesha mimba watakuwa tayari kulea watoto kwani wengi wao wamekuwa wakikataa ujauzito na wanaposhtaki polisi hawaoni hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya wanaume.
Kauli ya RPC
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Justus Kamugisha anasema kuwa kwa mwaka 2011-2012, zaidi ya watoto wanane wachanga walikutwa wametupwa wamekufa na wengine wakiwa hai na kuongeza kuwa watuhumiwa watano walifikishwa mahakamani.
 Wengine wamehukumiwa kifungo na kesi nyingine zimefutwa kwa kukosekana ushahidi na sababu mojawapo kubwa ni kutokana na jamii kutokusaidia kutoa ushirikiano Polisi wakati wa upelelezi.
 Kamanda Kamugisha anaitaka jamii kushirikiana  na polisi kuwafichua wale wanaobeba mimba na kisha kutoa mimba au kuua  watoto wao ili wachukuliwe hatua zi kisheria.
Anaeleza kuwa jamii ndiyo ipo karibu na wahusika wa tukio, wamekuwa hawako wazi kuwafichua waovu, jambo ambalo linawapa ugumu polisi wakati wa upelelezi wao, kiasi kwamba wengine huficha watuhumiwa.

0 comments: