WANAOJIHUSISHA NA TINDIKALI KUKOMESHWA. HIKI NDICHO ALICHOKISEMA RAISI KIKWETE
0
RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali yake imedhamiria na itahakikisha
inalimaliza tatizo la watu kumwagiwa tindikali, iwe ni Visiwani Zanzibar
au Tanzania Bara. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Rais Kikwete
amesema hivi karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni katika mitaa
ya Zanzibar na kukamata watu 10 wanaodaiwa kushiriki katika mipango ya
kuandaa na kutekeleza matukio ya watu kumwagiwa tindikali.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es
Salaam, ilisema Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi jijini New York
Marekani, alipokuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban
Ki Moon, baada ya kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa kutaka ufafanuzi wa
suala hilo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, chanzo cha tatizo la watu kumwagiwa
tindikali lina sura nyingi, lakini kutokana na jinsi Serikali
ilivyojipanga, tatizo litafikia mwisho baada ya siku chache.
“Ni kweli tumekuwa na vitendo hivyo, zaidi Visiwani Zanzibar kuliko Tanzania Bara ambako nako pia vimekuwapo vitendo hivyo.
“Ni jambo la kulaaniwa sana na hivi karibuni Jeshi la Polisi lilifanya
operesheni maalumu na msako mkubwa Tanzania Visiwani ambako watu 10
walitiwa mbaroni na watafikishwa katika vyombo vya sheria baada ya
taratibu za kisheria kukamilika.
“Wakati tatizo hili lilipoanza, tulidhani kuwa alikuwa ni Sheikh Soraga
aliyekuwa anatafutwa peke yake na watu ambao walikuwa hawakubaliani
kisiasa na msimamo wake, lakini mara wakaanza kushambuliwa watu wengine
wakiwemo wasichana wawili wa Uingereza ambao walikuwa wanafanya kazi za
kujitolea tu, lakini, tatizo hili ni lazima likome,” alisema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali wakati baadhi ya wananchi wameshadhurika kwa tindikali.
Miongoni mwao ni kiongozi maarufu wa Kiislamu Visiwani Zanzibar, Sheikh
Soraga ambaye alimwagiwa tindikali wakati akifanya mazoezi ya viungo
katika mitaa ya mji wa Unguja.
Mbali na huyo, viongozi wengine wa kidini wa Kanisa Katoliki visiwani
humo, wameshamwagiwa kemikali hiyo na pia wasichana wawili raia wa
Uingereza waliokuwa wakifanya kazi za kujitolea Visiwani Zanzibar, nao
walimwagiwa kemikali hiyo.
Wasichana hao baada ya tukio hilo lililotokea mwezi uliopita,
walisafirishwa kutoka Zanzibar na kuletwa Dar es Salaam kisha
wakasafirishwa kwenda nyumbani kwao Uingereza kwa ajili ya matibabu
zaidi.