TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: KUHUSU MAANDAMANO YA AMANI YA CHAMA CHA WANANCHI CUF.

0


THE CIVIC UNITED FRONT(CUF- Chama Cha Wananchi) 
TAREHE 29 JUNI 2013.
Waheshimiwa waandishi wa habari, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya uongozi wote wa kitaifa wa Chama chetu, naomba kuchukua fursa hii kuwakaribisha Ofisi Kuu ya chama ili tupate fursa ya kuzungumza nanyi na kwa maana hiyo kuzungumza na watanzania kupia kwenu ili ujumbe uliokusudiwa na chama uweze kuwafikia wananchi popote pale walipo.
Tumewaita leo tarehe 22 Juni 2013 tukiwa na agenda moja kuu nayo ni kuwaeleza kwamba Chama cha Wananchi CUF kimeandaa Maandamano ya Amani siku ya tarehe 29 Juni 2013 maandamano ambayo yataanzia eneo la Buguruni kituo cha Mafuta saa nne kamili asubuhi, kupitia barabara ya Uhuru, Mnazimmoja, Bibi Titi, Posta mpya , Aridhi hadi Ikulu.



Maandamano hayo ambayo yataongozwa na Mwenyekiti wa Chama taifa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, yanatarajiwa kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au mwakilishi wake, na kwamba yanalengo la kufikisha malalamiko ya wananchi kutokana na vitendo vya ukatili vinavyofanywa na jeshi la polisi na jeshi la wananchi ambalo kimsingi taifa letu linaelekea mahali pabaya.
Waheshimiwa waandishi wabari, mtakumbuka tarehe 15 Juni 2013 wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema wakihitimisha mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata nne za Arusha, palitokea mlipuko wa bomu uliopoteza maisha ya wananchi wane kwa mujibu wa taarifa za polisi na wengine wengi kujeruiwa vibaya.
Kwa kuwa jambo hili lipo katika hatua za uchunguzi, Chama cha CUF hakikusudii kuingilia uchunguzi unaoendelea lakini tunataka kufikisha ujumbe kwa rais kwamba hii si mara ya kwanza kuundwa kwa tume mbalimbali za uchunguzi hapa nchini. Kinachotusikitisha ni kuwa hata mara baada ya uchunguzi huo, hakuna ripoti inayotolewa hadharani kuonyesha chanzo cha tukio, wahusika na hatua zilizo au zinazotarajiwa kuchukuiliwa.
Tutamtaka Mheshimiwa rais kuhakikisha ripoti ya uchunguzi itokanayo na maafa yaliyotokea Arusha iwekwe wazi na serikali iwachukulie hatua stahiki wale wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo ili iwe funzo kwa wengine au wale wenye kuwa na malengo yanayofanana na hayo kwa kuwa Tanzania ni yetu sote na haitowezekana watu wachache wayachezee maisha ya watu kwa sababu ya kukidhi matakwa binafsi ambayo hayana tija kwa jamii.
Maandamano pia yanalenga kuishinikiza serikali kukomesha vitendo vya kinyama, vitendo vya kijangili vinavyofanywa na Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwakamata, kuwatesa, na kubaka wananchi wasio na hatia wa Mkoa wa Mtwara na hasa wanaoishi katika wilaya za Mtwara Mjini, MtwaraVijijini, na Newala huku baadhi yao wakichomewa nyumba zao moto na wengine wakiporwa mali zao. 
Waheshimiwa waandishi wa habari, mtakumbuka hivi karibuni pamekuwa na fukuto la suala la gesi katika Mkoa wa Mtwara ambapo baadhi ya maafisa wa Serikali wamekuwa wakipotosha madai ya wananchi ikidaiwa kwamba wananchi wa mkoa huo wamesema hawako tayari kuona gesi yao inatumiwa na wananchi wengine kinyume na wale wa mikoa ya Lindi na Mtwara jambo ambalo si kweli lakini wanayafanya haya ili kuwajengea chuki dhidi ya watanzania wengine ionekane kwamba wananchi wa Mtwara na Lindi ni wabinafsi na wasioitakia mema nchi yetu.
Madai ya wananchi wa Mtwara yanatokana na uzoefu waliokuwa nao katika maeneo yote ambapo pana miradi ya kimaenedeleo itokanayo na maliasili ya nchi, maeneo hayo yamekuwa masikini na watu wachache wamekuwa wanatajirika, walichotaka kufahamu wananchi watanufaikaje na uwepo wa gesi katika maeneo yao kabla ya kuinufaisha nchi mzima kwa kuwa wao ndiyo watakuwa wa kwanza kuathirika ikiwa patatokea hitilafu yoyote itokanayo na uchimbwaji wa gesi hiyo.
Leo tunaweza kujifunza kutokana na uchimbaji wa Dhahabu Geita (GGM), uchimbaji wa Almasi Mwadui Shinyanga, Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Nyamongo na maeneo mengine mengi, nini hali ya maisha ya wananchi wa maeneo hayo.
Pamoja na upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na watendaji wa serikali juu ya suala la gesi ya Mtwara, inashangaza hata Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambalo lilionekana awali kutenda haki kwa wananchi wa Mtwara baada ya wananchi kukosa imani dhidi ya Polisi kutokana na wizi na uporaji wa mali za wananchi huku wakichoma moto baadhi ya maduka kwa lengo la kuhalalisha vitendo vya hujuma pamoja na kuchoma moto soko la Nkana Read, Jeshi lililojijengea heshima kwa jamii nalo limeanza kuingia mkumbo wa kuwatesa raia bila makosa.
Mwanzoni mwa wiki hii Mkurugenzi wetu wa siasa wa wilaya ya Mtwara Mjini Mhe. Saibogi ambaye pia ni mwenyekiti wetu wa serikali ya Mtaa alitekwa na wanajeshi na kumpeleka katika Kambi yao iliyopo barabara ya kwenda Nanyamba ambapo walimvua nguo na kumpiga mijeredi usiku kucha bila hatia na kumuachia asubuhi yake huku wakiahidi kuwakamata viongozi wengine wa CUF ili kutoa funzo kwa wale wanaopigania haki za wananchi.
Matukio ya namna hii si ya kuyafumbia macho na yanatengeneza serikali yenye kiburi isiyotokana na maamuzi ya raia. Maisha ya namna hii hayawezi kuendeshwa katika nchi inayojiita huru kama yakwetu na badala yake mambo haya yanatukumbusha enzi za utawala wa kikoloni ambpo CUF kamwe hatupo tayari kuruhusu vitendo vya kishenzi kuona vinafanyika nchini petu.
Tulikianzisha Chama hiki kwa madhumuni ya kuwaunganisha watanzania wote popote walipo, bila kujali itikadi zao, waweze kukataa aina yoyote ya uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji, ubaguzi na udhalilishaji wa kisiasa au kiuchumi.
Aidha tuna dhamira ya kulinda, kutekeleza na kuzienzi haki za Binadamu pamoja na kuinua uchumi wa nchi kwa siasa zitumikie uchumi badala ya uchumi kutumikia siasa kama inavyofanyika hivi sasa. CUF tunaamini katika siasa za ustaharabu ambazo zitatuwezesha kuwa na jamii salama yenye mshikamano na ushirikiano katika kuijenga nchi yetu, lakini wenzetu wanatumia upole wetu na ustaharabu wetu kutufanyia vitendo vinavyokiuka utu wa mtu na hatimaye kila aliyepewa mamlaka ya kuongoza sehemu ya nchi yetu anageuka kuwa mfalme na kuamrisha kamata Yule, mpe kesi Yule na mwache Yule. Uvumilivu wetu usiwe mtaji kwa CCM na serikali yake kutufanya watakalo, nasi ni binadamu.
Waheshimiwa waandishi wa habari, maandamano yetu yanalenga pia kuitaka serikali kuwasikiliza wananchi wa Mtwara kwa kukaa nao chini, kujua hoja zao na kutoa ufafanuzi pale patakapobidi, sisi tunaamini wanazo hoja za msingi na wakisikilizwa serikali itaona namna ya kuzifanyia kazi hoja hizo badala ya kukurupuka na kutoa kauli za kibabe eti hawa wanachochewa na vyama vya siasa au pana watu wasioitakia mema nchi ndiyo wanachochea, kauli hizi zinajenga chuki na zanakosa uzalendo wa taifa. Haiwezekani hao wanaojiita ndiyo wazalendo halisi wawe wanaifidi nchi alafu tuendelee kukaa kimya kama vile wananchi wa kusini ni watu wasioweza kufikiri na kupambanua baya na zuri.
Wakati wananchi hawa walipopeleka maombi yao kupitia kwa Mhe. Mohamedi Habibu Mnyaa Mbunge wa Mkanyageni, ilikuwa nafasi nzuri kwa serikali kuweza kusikiliza maombi yao na kutoa maamuzi, badala yake siasa zikatumika, maombi yakakataliwa leo Bunge linaunda kamati ya uchunguzi iende mtwara wakachunguze nini ikiwa tayari hoja zao zilikataliwa?
Ieleweke kuwa nchi yetu itajengwa na watanzania wenyewe kwa kushirikiana na kusikilizana. Amani ya kweli itapatikana ikiwa haki itaonekana kutendeka kwa jamii yote. Waheshimiwa waandishi wa habari, haya ni sehemu tu ya mambo ambayo tunakusidia kumfikishia rais wetu ili aweze kuyafanyia kazi.
Mungu Ibariki CUF, Mungu ibarika Tanzania.
Imetolewa na Shaweji Mketo, 
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa, tarehe 22 Juni 2013.

0 comments: