ZIJUE SABABU ZA RAIS OBAMA KUTOKWENDA KENYA, NIGERIA
0
Rais Barack Obama. |
Rais Barack Obama amepongeza hatua zilizopigwa na Afrika katika kujenga demokrasia, imeelezwa kutoka Dakar, Senegal.
Obama alisema jana baada ya kukutana na Rais Macky Sall wa Senegal alikowasili juzi usiku ukiwa ni mwanzo wa ziara yake ya nchi tatu za Afrika, Tanzania ikiwamo.
Alisema Senegal ni moja ya wabia wakubwa wa Marekani katika bara la Afrika na inaonekana kuwa mfano wa utawala bora. Nchi zote anazotembelea – Senegal, Afrika Kusini na Tanzania- zina demokrasia ya kweli.
Katika ziara yake hiyo nchi za Kenya ambako baba yake alizaliwa na Nigeria ambayo inaongoza Afrika kwa uzalishaji mafuta jamii ya petroli lakini imekumbwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu, hatazitembelea.
Maofisa wa Serikali walisema kutuhumiwa kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) jijini The Hague, kutokana na ghasia za uchaguzi, ndiko kumesababisha ugumu wa Obama kupita nchi hiyo.
Ziara yake nchini Afrika Kusini, inatarajiwa kugubikwa na hali mbaya kiafya aliyonayo Rais wa zamani Nelson Mandela.
Hata hivyo, Ikulu ya Marekani, imesema itafuata kitakachoamuliwa na familia ya Mandela ya kama ana uwezo wa kumpokea Obama akiwa hospitalini.
Obama na Mandela walikutana mwaka 2005, wakati Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alipokwenda Washington, DC, kipindi Obama akiwa ndiyo kwanza amechaguliwa useneta, ambapo wawili hao tangu wakati huo walikuwa wakiwasiliana kwa simu.
Lakini matarajio ya muda mrefu ya viongozi hao wawili wa kwanza weusi wa Afrika Kusini na Marekani kukutana, sasa yanaonekana kushindikana.
Obama alisema Afrika imepiga hatua kubwa katika kufanikisha demokrasia, akizitaja Senegal, Ghana, Sierra Leone, Ivory Coast na Niger.
“Senegal ni moja ya mataifa yenye demokrasia katika Afrika na moja ya wabia wakubwa tulionao katika eneo hili la Afrika. Inaelekea pazuri na mabadiliko ya kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kama ilivyo, Waafrika wengi hivi sasa wameamka kudai serikali zao ziwajibike na kusaidia watu, naamini Senegal inaweza kuwa mfano katika hilo,” alisema Obama.
“Haitoshi kuwa na uchaguzi, haitoshi kuwa na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia. Mnahitaji kuwa na mahakama huru. Mnatakiwa kuwa na imani kwa utawala wa sheria. Mnahitaji kuwa na jitihada za kupambana na rushwa,” Mshauri wa Obama wa Sera ya Mambo ya Nje, Ben Rhodes alikaririwa akisema.
“Mnahitaji kuwa na juhudi za kupambana na rushwa kwa sababu, kusema kweli, si nzuri tu kwa demokrasia na heshima kwa haki za binadamu, lakini ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Afrika.”
Rais huyo wa Marekani anasafiri katika kivuli cha watangulizi wake, Bill Clinton na George W. Bush, ambao wanakumbukwa kwa mipango yao ya maendeleo ya uchumi na mapambano dhidi ya Ukimwi.
Baada ya kuzuru Goree jana akifuatana na mumewe, Michelle pia atazuru shule ya kati ya wasichana ya Martin Luther King akifuatana na mke wa Rais Sall.
Jumapili atatembelea kisiwa cha Robben ambako Mandela alifungwa kwa miaka 18 kati ya 27 aliyokaa gerezani. Hata hivyo, bado hakuna uhakika kama ziara hiyo itafanyika kutokana na hali ya Mandela kuendelea kuwa mbaya.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, amesema ziara ya Rais Obama haitaathiri shughuli za kiuchumi wala kuzuia watu kuingia na kutoka jijini.
Amebainisha kuwa Obama atakapowasili nchini atatembelea na kuzindua barabara ya Ocean ambayo Manispaa ya Ilala imepanga kuibadili jina na kuipa jina la Barack Obama Avenue ikiwa ni heshima kwake.
Pia gazeti hili limeshuhudia maandalizi ya mapokezi ya kiongozi huyo, ambapo barabara kadhaa zinazoaminika kuwa atazitumia katika ratiba yake zinafanyiwa ukarabati kwa kuwekwa lami na taa.
Akizungumza na mwandishi Dar es Salaam jana Sadiki, alitaka wakazi wa Dar es Salaam, waitumie vyema fursa ya ujio wa kiongozi huyo nchini na kuachana na maneno ya mitaani kwamba shughuli zote za kiuchumi zitasimama.
Kuhusu baadhi ya wafanyabiashara wadogo kuondolewa katika maeneo yao, Sadiki alisema suala hilo halihusiani na ziara hiyo na kwamba ni mpango wa Jiji wa muda mrefu kulirejesha katika usafi.
Aidha baadhi ya vyombo vya ulinzi kutoka Marekani vimeanza kuonekana jijini, ambapo manowari ya Marekani ilionekana ikiwa imeegeshwa pembeni mwa kisiwa cha Mbudya.