APATA KIPIGO HADI KUFA KISA KUMFOKEA HAWARA WA MUMEWE

0

  


 Kamanda wa polisi Katavi,Dhahiri Kidavashari

MKAZI wa Kijiji cha Itetemya katika Tarafa ya Karema mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda mkoani Katavi , Nyingi Shida (21) anadaiwa kuuawa na mumewe baada ya kumpiga na kumvunja shingo yake kisha kumtundika mtini.
Inadaiwa mume wa marehemu huyo alimuua mkewe baada ya kuchukizwa na kitendo cha mkewe huyo kwenda kumfokea mwanamke ambaye inadaiwa kuwa ni ‘hawara’ yake .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alimtaja mshitakiwa kuwa ni Masanja Kulwa (23) mkulima kijijini humo ambaye baada ya kumvunja shingo alimfunga na kipande cha chandarua shingoni mwake na kumning’iniza mtini mita 70 kutoka nyumbani kwao.
Tukio hilo lilitokea Julai 31 , mwaka huu saa 6:00 usiku kijijini humo baada ya wanandoa hao kuzozana na kushutumiana ambapo Shida anadaiwa kukasirishwa na tabia ya mumewe kuwa na mahusiano na mwanamke kijijini humo ambaye pia ni jirani yao.
Akisimulia mkasa huo , Kidavashari alidai siku moja kabla ya tukio hilo kutokea marehemu akiwa amejifunga ‘kibwebwe’ alikwenda nyumbani kwa mwanamke mwezake kijijini humo usiku na kumuonya akome kuendelea na mahusiano ya kimapenzi na mumewe vinginevyo ataona ‘cha mtema kuni ‘.
“Siku iliyofuata mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa ni ‘hawara’ yake alimsimulia jinsi alivyofokewa na mkewe, ndipo wanandoa hao walianza kuzozana huku mume akimshutumu mkewe kwenda kumfokea ‘ hawara yake,” aliongeza.
Inadaiwa ndipo wanandoa hao waliposhindwa kuelewana na kuanza kupigana ambapo alfajiri ya siku iliyofuata wapita njia waliuona mwili wa marehemu ukiwa unaning’inia mtini akiwa ameshakufa ambapo mara moja walimsaka mumewe na kumkamata kisha kumkabidhi katika Kituo cha Polisi.
Uchunguzi wa kitabibu ulibainisha kuwa shingo ya marehemu huyo ilikuwa imevunjika huku akiwa na majeraha yaliyotokana na kipigo katika sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo alionekana kuwa na majeraha makubwa mdomoni.
Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote mara baada ya uchunguzi wa awali wa shauri hilo la mauaji kukamilika.

0 comments: