MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI 'ABSALOM KIBANDA' ALONGA

0

 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini Tanzania (TEF), "Absalom Kibanda" amesema zipo taarifa mbalimbali za kutaka kupotosha ukweli kuhusu yeye, lakini ukweli utabaki kuwa kweli na tukio alilofanyiwa ni la kihalifu, linalotokana na misimamo ya kazi yake.

Aidha amesema kabla ya kushambuliwa na kujeruhiwa vibaya alikuwa muoga sana na kwamba hakupata kujua kama yeye ni jasiri kwa kiwango hicho.

Kibanda alisema hayo jana wakati akizungumza Dar es Salaam katika kipindi cha Jenerali On Monday na kuongeza kuwa kalamu yake ndiyo iliyomfikisha hapo na kwamba bado atajisemea mwenyewe huku akisema kweli daima.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari Limited (2006), alijeruhiwa vibaya katika mkasa uliotokea Machi 6, mwaka huu na kumwacha na ulemavu wa jicho, kidole na mifupa kadhaa mwilini kuvunjika.

“Nilikuwa muoga sana kabla ya kupatwa madhala haya, nilikuwa nikiwaza jambo mara mbilimbili na sikupata kujua kama mimi ni jasiri kiwango hiki…kwani hata maneno ya madaktari waliokuwa wakinihudumia yalinifariji kuwa hata shinikizo la damu na sukari viko katika hali nzuri,” alisema Kibanda na kutaka uchunguzi zaidi ufanyike.

Alisema zipo taarifa mbalimbali za kutaka kupotosha ukweli kuhusu yeye lakini ukweli utabaki kuwa kweli na kwamba yapo mambo ambayo atayafanya tofauti na ilivyokuwa awali.

“Katika miezi mitatu niliyokuwa nikipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini zipo lugha nyingi za kishabiki ziliandikwa…ni wakati wa kuchunguza kwa kina na kusema ukweli,” alisema Kibanda na kuongeza kuwa leo (jana) ni siku 100 tangu alipofanyiwa tukio hilo, lakini hakuna aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani. Kuhusu kupata ushirikiano katika shauri lake, alisema amekuwa akipata mawasiliano kutoka kwa viongozi mbalimbali wakiwemo pia viongozi wa ulinzi na usalama wa Taifa ambao wanachunguza suala hilo.

“Maofisa wa polisi wamekuwa wakiwasiliana nami na hata nilipokuwa Afrika Kusini Jeshi la Polisi lilimtuma ofisa wake na alifanya mahojiano nami kuhusu tukio hili,” alisema Kibanda na kusisitiza kuwa ifikie wakati serikali iwe inajali pindi yanapotokea matukio ya aina hiyo.

Aidha alisema tukio alilofanyiwa ni la kihalifu na anaamini kuwa aliumizwa kwa misimamo yake ya kazi, lakini bado anatoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuchunguza tukio hilo.

Kibanda alisema yapo mambo ambayo yalipindishwa kuhusu tukio hilo na kwamba atajisemea mwenyewe.

Akihitimisha kipindi hicho, Muandaaji, Jenerali Ulimwengu alisema matukio kama hayo yanapotokea yana tabia ya kukua, kusambaa na mwishowe kuota meno marefu na kuyaondoa huwa hayawezekaniki tena, hivyo matukio kama hayo yazuiwe yasijirudie.

0 comments: